. 

CHADEMA ngangari, Mbinu za CCM zagonga mwamba

No Comments

 
KUIMARIKA kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kunazidi kuwachanganya viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaotumia mbinu mbalimbali kukidhoofisha.
Tanzania Daima Jumapili imedokezwa kuwa licha ya viongozi wa CCM kuvitumia vyombo vya dola kuzima kasi ya CHADEMA, bado mambo yanaonekana kukiendea mrama chama tawala.
Hali ya mambo inaonesha kuwa CHADEMA inainyima usingizi CCM na serikali yake, ndiyo maana hivi sasa wameamua kukipaka matope kwa kutumia mbinu mbalimbali kuwafungulia kesi za ugaidi makada wao.
Uchambuzi wa kina wa matukio ya kisiasa ya hivi karibuni uliofanywa na gazeti hili umebaini kuwa kwa sasa CCM inakabiliwa na wakati mgumu kisiasa kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya chama hicho.
Kuna viashiria vya wazi kuwa enzi za CCM kutawala siasa za Tanzania zinaelekea ukingoni kadiri CHADEMA inavyoimarika.
Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa CCM imeamua kulitumia Bunge na vyombo vya dola, ikiwamo polisi kufanikisha azima yao ya kuidhoofisha CHADEMA.
Jeshi la Polisi limekuwa likituhumiwa na viongozi wa CHADEMA na wananchi kuwa linatumiwa kuanzisha vurugu zinazosababisha mikutano ya CHADEMA kuvurugika au kutokea vurugu.
Vurugu hizo zinaelezwa ni mipango maalumu ya kukipaka matope chama hicho kikuu cha upinzani nchini mbele ya umma ili wasikichague kwenye chaguzi zitakazofanyika mwakani na mwaka 2015.
Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya siasa wameanza kupata hofu juu ya mwenendo wa Jeshi la Polisi katika mikutano ya CHADEMA ambayo mara nyingi risasi na mabomu ya machozi hutumika.
Agosti 27, mwaka jana polisi walizuia na kuwatawanya wafuasi wa CHADEMA waliokuwa wakielekea kwenye mkutano uliopigwa marufuku.
Katika purukushani hiyo kijana mmoja aliyekuwa akiuza magazeti mjini Morogoro aliuawa kwa risasi ingawa polisi walidai alipigwa na kitu kizito nyuma ya kichwa chake.
Septemba 2, jana mkoani Iringa, polisi walitumia mabomu ya machozi na risasi kukabiliana na wafuasi wa CHADEMA na mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi, alilipuliwa na bomu. 
Viongozi na wanachama wa CHADEMA walikusanyika katika ufunguzi wa tawi la chama chao katika Kijiji cha Nyororo, mkoani Iringa.
Kumekuwapo juhudi za makusudi za polisi na CCM kujaribu kuihusisha CHADEMA katika matukio yote mawili ya mauaji kwa lengo la kukichafua lakini bado upepo unaonekana kuvuma vibaya kwa watawala na vyombo vya dola.
Tanzania Daima, Jumapili, limedokezwa kuwa mkakati wa pili unaotumiwa na CCM dhidi ya CHADEMA ni kuwabambikiza kesi za ugaidi viongozi wake ili chama hicho kionekane hakifai mbele ya Watanzania. 
Machi, mwaka jana, Mkururgenzi wa Ulinzi na Usalama wa CHADEMA, Wilfred Lwakatare, alionekana kwenye mitandao ya kijamii akipanga kile kilichodaiwa na polisi na CCM kuwa mpango wa kumteka na kumdhuru Mhariri Mtendaji wa Mwananchi Communications, Denis Msacky.
Baadaye Lwakatare akashtakiwa mahakamani kwa tuhuma za ugaidi na kesi hiyo ikaanza kutumiwa kisiasa na makada wa CCM ili kuidhoofisha CHADEMA.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Mwigulu Nchemba, alikiri kufahamu watu walioiandaa video hiyo na kuiweka kwenye mitandao.
Kama ilivyokuwa kwa mipango mingine, mpango huu nao haukufua dafu baada ya Mahakama Kuu kumfutia Lwakatare mashtaka yote yaliyohusu ugaidi.
Kufutwa kwa mashtaka hayo kulikuwa pigo kubwa kwa CCM na polisi.
Harakati hizo zinaonekana kuzidi kushika kasi ambapo Juni 24 mwaka huu, makada wa CHADEMA wamefunguliwa mashtaka mengine ya ugaidi mkoani Tabora.
Makada hao wanatuhumiwa kumteka na kumdhuru kwa tindikali kada wa CCM wilayani Igunga mwaka 2011.
Washitakiwa hao ni pamoja na Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kilewo, Evodius Justinian wa Bukoba, Oscar Kaijage wa Shinyanga, Seif Magesa Kabuta wa Mwanza na Rajab Daniel Kihawa wa Dodoma.
Watuhumiwa hao walisomewa shitaka la ugaidi kwa madai ya kumteka na kummwagia tindikali kada wa CCM, Musa Tesha, katika kampeni za uchaguzi mdogo wa Igunga uliofanyika mwaka 2011.
Juni 15, mwaka huu kulitokea mlipuko wa bomu katika mkutano wa CHADEMA wa kufunga kampeni za uchaguzi wa madiwani mkoani Arusha, ambapo watu wanne waliuawa na zaidi ya 70 kujeruhiwa.
Mara baada ya mlipuko huo viongozi wa CCM wamekuwa wakiihusisha CHADEMA na tukio hilo huku CHADEMA wakidai polisi na serikali ya CCM ndio wahusika wakuu.
Tukio hilo lilianza kuchukua mwelekeo wa kisiasa huku CCM wakionekana kutaka CHADEMA idhibitiwe katika mikutano yake ambayo imekuwa ikisababisha vifo na majeruhi.
Hata hivyo Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alisema wanao ushahidi unaomuonesha aliyerusha bomu alikuwa ni askari na alilindwa na wenzake wakati akitoka uwanjani hapo.
Katika mwendelezo wa kuibana CHADEMA kwa kuwafungulia makada wake kesi zisizo na msingi, juzi polisi walimshtaki mahakamani Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, kwa tuhuma za kumtukana Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.
Polisi walidai kuwa Mbilinyi maarufu kama Sugu alisambaza katika mtandao wa kijamii wa facebook ujumbe wa kumtusi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, baada ya kauli yake kwamba: “Wanaokaidi amri ya polisi wapigwe tu,” kuwa ni upumbavu.
Hata hivyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Dodoma ilitupilia mbali shtaka kutokana na hati ya mashtaka kukosa maelezo ya kutosheleza kuonesha kosa lililotendwa na Sugu, hivyo hati hiyo kukosa nguvu za kisheria.
Aidha, katika kuthibitisha kuwa viongozi wa CCM wamechanganywa na nguvu na ushawishi wa CHADEMA, uongozi wa Bunge nao umezidisha harakati zake za muda mrefu za kuwabana wabunge wa chama hicho kwa kuwazuia kuvaa suti za kombati ndani ya Bunge.
Kuzuiwa kwa mavazi hayo ambayo sasa yanatafsiriwa kuwa mavazi ya chama hicho, kunaelezwa ni ukiukwaji wa kanuni za Bunge.
Licha ya mbinu zote hizo, CHADEMA hivi sasa inaonekana kuimarika zaidi kwani katika uchaguzi wa udiwani uliofanyika hivi karibuni ilifanikiwa kuipoka CCM kata tatu.
Matokeo hayo yanatoa ishara kuwa uchaguzi wa serikali za mitaa utaofanyika mwakani na ule mkuu utakaofanyika mwaka 2015, hali itakuwa ngumu zaidi kwa CCM.
Wadadisi wa masuala ya siasa wameweka wazi kuwa CCM imo katika hali ngumu kisiasa na haitashangaza kuiona ikishindwa vibaya katika uchaguzi mkuu ujao wa rais, wabunge na madiwani utakaofanyika mwaka 2015.
Kama CCM itashindwa katika uchaguzi mkuu ujao, basi itakuwa imefuata njia iliyopitwa na vyama vingine vikongwe katika Bara la Afrika, vilivyopigania uhuru wa nchi zao na ambavyo vimeondolewa madarakani na wanamageuzi kuanzia miaka ya 1990.
Vyama vikongwe Afrika vilivyowahi kuangushwa na wanamageuzi ni pamoja na chama kilichopigania uhuru wa Zambia cha UNIP chini ya Dk. Kenneth Kaunda, Chama cha Malawi Congress (MCP), kilichoongozwa na hayati Dk. Kamuzu Banda na Chama cha KANU kilicholeta uhuru wa Kenya, chini ya hayati Jomo Kenyata, ambacho kilitimuliwa madarakani mwaka 2002.